KKOOAPP

Sera ya Faragha

Nini KKOOAPP inakusanya, kwa nini, na nani anaweza kuiona.

Ilisasishwa tarehe 17 Septemba 2026

Tunachokusanya

Namba yako ya simu, ambayo ndiyo unayotumia kuingia.

Jina na picha unayochagua kwa wasifu wako, na chochote kingine unachoongeza, kama anwani ya duka au kiungo cha mitandao ya kijamii.

Matangazo yako: vichwa, maelezo, bei, picha, na wilaya, kata au alama ya ramani unayoiambatanisha.

Ujumbe na bei unazotuma kupitia programu, na uliyemtumia.

Matangazo unayohifadhi na wauzaji unaowafuata.

Lugha ya simu yako, ili programu ifunguke kwa Kiswahili au Kiingereza.

Eneo

Wewe unachagua wilaya, na unaweza kuweka alama ya ramani kwenye tangazo. Ukiruhusu, programu pia hutumia eneo la simu yako kupanga matangazo kwa ukaribu.

Alama unayoweka kwenye tangazo huonwa na yeyote anayefungua tangazo hilo, kwa hiyo iweke karibu na mahali mtakapokutana, si mlangoni kwako.

Unaweza kukataa ruhusa ya eneo na bado ukatumia programu. Utachagua wilaya kwa mkono badala yake.

Watu wengine wanachokiona

Jina lako la kuonekana, picha, matangazo uliyo nayo hai, na muda uliokaa na akaunti.

Namba yako ya simu si ya hadhara. Inaonyeshwa tu kama umewasha chaguo la WhatsApp au la kupiga simu kwenye mipangilio yako, na unaweza kuizima tena.

Ujumbe ni kati yako na unayezungumza naye. Tunaweza kuusoma pale tunapohitaji kuchukua hatua kuhusu ripoti.

Hatuonyeshi matangazo ya biashara, wala hatuuzi au kukodisha taarifa zako kwa mtu yeyote.

Zinapohifadhiwa

Seva na hifadhidata yetu ziko Frankfurt, Ujerumani, na picha zinahifadhiwa na Cloudflare. Hii ina maana taarifa zako zinashughulikiwa nje ya Tanzania.

Misimbo ya kuingia hupitishwa kwa WhatsApp, inayoendeshwa na Meta, ambayo hushughulikia namba yako chini ya masharti yake yenyewe.

Tunazihifadhi kwa muda gani

Matangazo huisha muda siku 30 baada ya kuwekwa na yanaweza kurudishwa.

Ujumbe na bei huhifadhiwa wakati akaunti yako ikiwa wazi, ili mazungumzo unayorudia bado yawepo.

Unaweza kufuta akaunti yako kutoka kwenye wasifu wako wakati wowote. Wasifu wako unafutwa, matangazo yako yanaondolewa na picha zake zinafutwa, na namba yako ya simu inaachiwa ili uweze kuanza upya. Mazungumzo uliyokuwamo yanabaki kwenye kikasha cha mwenzako bila jina lako, yakionyesha bado jina la kitu, kwa sababu ni kumbukumbu yake ya biashara ambayo huenda hajaimaliza. Kuzuia na ripoti zinabaki, kwa sababu zipo kuwalinda wengine.

Uchaguzi wako

Unaweza kuhariri au kufuta tangazo wakati wowote, kubadilisha au kuondoa taarifa za wasifu wako, na kuwasha au kuzima njia za mawasiliano.

Unaweza kumzuia mtumiaji mwingine, jambo linalowaficha nyinyi kwa nyinyi.

Kufuta akaunti yako, fungua wasifu wako kisha chagua Futa akaunti. Hufanyika papo hapo na haiwezi kutenguliwa. Kuona tulichonacho kukuhusu au kukisahihisha, tuandikie support@kkooapp.com.

Watoto

KKOOAPP si kwa ajili ya watu walio chini ya miaka 18. Tukigundua kuwa akaunti ni ya mtoto, tutaiondoa.

Mabadiliko

Tukibadilisha jinsi taarifa zako zinavyotumika, tutasema ndani ya programu.

Maswali yaende support@kkooapp.com.